TANZANIA INAENDA KUSHIRIKI, SI KUSHINDANA.....!!!!

Mshindi wa Shindano la Miss Tanzania 2013, Happiness Watimanywa, Jumamosi ya wiki iliyopita, alikwea pipa kuelekea jijini London, Uingereza kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World, yanayotarajiwa kutimua vumbi Desemba 14, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Excel London.
Mshindi wa Shindano la Miss Tanzania 2013, Happiness Watimanywa.
MAANDALIZI HAFIFU
Hata hivyo, wakati Happiness akiondoka nchini, mama yake mzazi alikuwa akiendelea kunung’unika kwamba Kamati ya Miss Tanzania, ilishindwa kumfanyia mwanaye maandalizi ya kutosha kwa wakati ikiwa ni pamoja na kumcheleweshea fedha za kufanyia shopping pamoja na maandalizi mengine.
Akizungumza na kituo kimoja cha runinga, mama mzazi wa mnyange huyo, alisema wakati mwingine alilazimika kutoa fedha zake za mfukoni ili kumsapoti mwanaye, ikiwa ni pamoja na kumpa fedha kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kupiga picha zitakazotumika Miss World.

ATAFUA DAFU MBELE YA WENZAKE?
Happiness si mshiriki pekee kwenye mashindano hayo, atakuwa na kazi ya ziada ya kuchuana na wenzake 128 kutoka nchi mbalimbali duniani, kumsaka mrembo atakayerithi taji ambalo mpaka sasa linashikiliwa na mwanadada Megan Young wa Ufilipino.
Swali la kujiuliza ni je, Tanzania inategemea Happiness afanye vizuri wakati mpaka anaondoka, mwanadada huyo na mzazi wake walikuwa wakinung’unika kutokana na maandalizi hafifu aliyoyapata? Tunategemea atang’ara mbele ya wenzake ambao nchi zao zinawaandaa vya kutosha kwa kuwapa sapoti ya nguvu?
LUNDENGA APIGA KIMYA
Showbiz ilimtafuta Mkurugenzi wa Lino International, Hashim Lundenga, waandaaji wa shindano hilo ili kumuuliza ukweli kuhusu madai hayo lakini hakuwa akipokea simu yake licha ya mwandishi kumpigia mara kadhaa. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, bado aliendelea kupiga kimya (kuuchuna).
Happiness Watimanywa.
KAMATI YA MISS TANZANIA KUNANI?
Sakata la Watimanywa kuondoka bila kuwa na maandalizi ya kutosha, linakuja siku chache baada ya kutokea tukio lingine la kihistoria ambapo aliyekuwa mshindi wa kwanza mwaka huu kwenye mashindano hayo, Sitti Mtemvu alilazimika kuvua taji lake kwa madai ya kudanganya umri, na nafasi yake kuchukuliwa na mshindi wa pili, Lilian Kamazima.
USHAURI KWA HAPPINESS
Japokuwa umeondoka katika mazingira magumu, Watanzania wengi wanakutazama kwa macho ya matumaini kwamba angalau unaweza kuwatoa kimasomaso kwenye mashindano hayo makubwa zaidi katika tasnia ya urembo duniani.
Showbiz inakutakia kila la heri Happiness, jiamini kwamba unaweza kufanya makubwa na kurudisha heshima nyumbani, kama alivyowahi kufanya Nancy Sumari kipindi hicho. Licha ya ‘magumashi’ ya Kamati ya Miss Tanzania, amini kwamba Watanzania wapo nyuma yako!- Mhariri.
Previous
Next Post »