Hatimaye
wajumbe wa Mkutano wa 36 wa Bunge la SADC ambalo linaloundwa na mabunge
ya nchi wanachama wa SADC (SADC PF) wamemchagua kwa kishindo Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda kuwa Rais
wa Bunge hilo kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.
Makinda
ambaye alikuwa hana mpinzani katika uchaguzi huo, aliungwa mkono na
wajumbe wote wa Mkutano huo ambao ni Maspika na Wabunge kutoka mabunge
ya Nchi wanachama wa SADC jana tarehe 2 Novemba, 2014 wakati wa
kuhitimisha Mkutano wa 36 wa Jukwaa la Mabunge ya SADC uliokuwa
ukifanyika katika Hotel ya Elphant Hii iliyopo Mjini Victoria Falls
Nchini zimbabwe.
Msimamizi wa
uchaguzi ambaye ni Katibu Mkuu wa Bunge la SADC Dkt. Esau Chiviya
alisema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za Bunge hilo, kanuni ya Kanuni
ya 42 (2) i inatamka wazi kuwa endapo kutakuwa na mgombea mmoja pekee,
basi atawahoji wajumbe na endapo watamkubali basi atamtangaza rasmi
kuwa amechaguliwa kushika nafasi hiyo.
“ Kwa kuwa
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda hana mpinzani na kwa kuwa
nimewahoji na wote mmemuunga mkono, basi natangaza kuwa ndiye Rais mpya
wa Bunge la SADC kwa miaka miwili ijayo”. Alitangaza Dkt. Chiviya
Awali kwa
mujibu wa utaratibu wa uongozi ndani ya chombo hicho, Makinda alitakiwa
kugombea nafasi hiyo pamoja na Spika wa Ushelisheli na Msumbiji ambao
wote kwa pamoja hawakushiriki uchaguzi huo na kuamua kumuunga mkono
Spika Makinda
Akisoma
hotuba yake ya shukrani kwa wajumbe wa Mkutano huo, Mhe. Makinda
amewashukuru wajumbe wote walioshiriki katika uchaguzi na kumuunga mkono
ili aweze kuwaongoza katika kipindi kingine cha miaka miwili.
“ Ninalo deni
kubwa kwenu kwa jinsi mlivyoniunga mkono na kama mnavyojua jukumu letu
kubwa mbele yetu ni kuwa na Bunge imara la SADC jambo ambalo
nawahakikishia kwa pamoja tutafanikiwa
Makinda
alisema kama mnavyojua, malengo makuu ya SADC PF ni kuwa na Bunge la
kikanda litakalowakilisha mawazo ya pamoja kutoka kila Bunge la Nchi
wananchama wa SADC, hili ndilo lengo kuuu la waasisi wa umoja huu
walilokusudia wakati wa kuanzisha chombo hiki mwaka 1997 hivyo nasisi
lazima tulienzi na kulitekeleza.
Mhe. Makinda
amesisitiza kuwa kwa miaka 17 iliyopita ya uhai wa Bunge hili la SADC
wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutimiza malengo yake kama
ilivyojiwekea katika Katiba yake ambayo ni kukuza na kuimarisha utawala
wa kisheria, Kusimamia Masuala ya usawa wa Kijinsia, Utawala bora,pamoja
na kukuza demokrasia katika ukanda wa SADC.
Aidha
aliwakumbusha wajumbe na wanachama wa Bunge hilo kuwa, anachukua nafasi
hiyo huku Bunge hilo likikabiliwa na changamoto lukuki za kiutendaji
ambazo nyingine ni za kimuundo, kiuchumi na za kimkakati.
“Bado kuna
haja ya kutatua changamoto mbalimbali ndani ya Bunge letu hususani
Ukosefu wa namna bora ya kuwasilisha maamumizi ya Bunge hili ndani ya
Utaratibu wa Jumuiya ya Wanacham wa nchi za SADC, Uwajibikaji hafifu
kuhusu maamuzi ya Bunge hili kwa nchi wanachama, ukosefu wa namna bora
ya kushirikiana na Bunge la Afrika, mawasiliano hafifu kati ya Chombo
hiki na Mabunge ya Nchi wananchama, Uhaba wa rasilimali watu na fedha za
kuendeshea chombo hiki. Alisema Makinda
Mkutano wa
huo wa Bunge la SADC umemalizika rasmi jana baada ya pia kuchaguliwa
makamu wa Rais wa Bunge hilo ambaye ni mhe. Njovya Lema Mbunge kutoka
Malawi.
Hakimiliki; 1999 ; 2014 Google
Hakimiliki; 1999 ; 2014 Google
ConversionConversion EmoticonEmoticon