JINA la Zari hivi sasa limekuwa jina maarufu katika masikio ya Watanzania, Afrika Mashariki na kwingineko hasa baada ya mwanadada huyo mfanyabiashara na mwanamuziki wa Uganda kuwa na urafiki na Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nassib Abdul maarufu kwa jina la usanii Diamond Platnum.
Zari The Lady Boss |
Uhusiano kati ya Zari na Diamond umezua gumzo kila eneo Tanzania na Afrika Mashariki huku wakifananishwa na mastaa wa nje kama vile Kanye West na Kim Kardashian kwa namna wanavyofuatana wakati wote huku Diamond akionesha kila aina ya mbwembwe za kumjali mrembo huyo kutoka Kampala, Uganda.
Uhusiano wa Zari na Diamond umewafanya kuandamana kila sehemu hivi sasa. Wawili hao walianza kuonekana kuwa na ukaribu wa mahusiano tangu Diamond alipokwenda Afrika Kusini kwenye Tuzo za Channel O ambapo Diamond aliibuka na ushindi wa Tuzo tatu.
Baada ya Tuzo hizo, Zari alimualika Diamond kushiriki katika ‘pati’ maarufu ambayo mwanadada huyo huandaa kila mwaka nchini Uganda ambapo mwaka huu ilijulikana kama All White Ciroc Party.
Wawili hao baada ya sherehe hiyo, walifuatana ambapo Zari alimsindikiza Diamond nchini Rwanda na Burundi alipokwenda kutoa burudani nchini humo, na picha kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kuwafanya wawili hao kuwa gumzo hivi sasa katika mitandao Tanzania na Afrika Mashariki.
Je, Zari ni nani hasa? Zarina Hassan Tlale.Maarufu kama Zari ni Mganda anayeishi Afrika Kusini.
Mrembo huyo ni mwanamuziki na mfanyabiashara. Ni mwanamke aliyefanikiwa na anayependa kuishi maisha ya kifahari. Anamiliki magari ya kifahari na yenye gharama kubwa kama Lamborghini Gallardo, BMW- 2006,Chrysler-2008, Audi Q7-2010 na Ranger Rover Sports .
Mwanadada huyo ni binti wa Halima Sultan Hassan na Nasur Hassan akiwa na asili ya damu mchanganyiko ikiwa ni pamoja na ya Kihindi , Toro, Somalia na Burundi kutoka mji wa Jinja, Uganda. Babu mzaa mama yake anatoka India na bibi yake ni kutoka Uganda. Babu yake mzaa baba ni kutoka Somalia na bibi yake mzaa baba anatoka Burundi.
Zari maarufu kama The Bosslady aliwahi kuolewa na mwanamume anayejulikana kwa jina la Ivan na kubarikiwa watoto watatu wa kiume Pinto, Didy na Quincy na anamiliki kampuni tatu.
Mwanadada huyu alizaliwa Septemba 23,1980. Zari amekulia katika mji wa Jinja katika nchi ya Afrika Mashariki inayojulikana kama Uganda.
Zari alisoma shule ya msingi, kisha kwenda Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jinja ambapo alisoma kwa bidii kutimiza ndoto zake. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, mwanadada huyo alihamia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala ambapo alikuwa akitoa burudani ya muziki katika maeneo ya starehe kabla ya kuhamia mjini London, Uingereza na kusomea Stashahada ya masuala ya urembo (cosmetology).
Historia yake kimuziki inaonesha Zari alianza kuimba akiwa na umri mdogo wakati akisoma shule ya msingi ambapo alikuwa akitoa burudani katika matamasha ya muziki yaliyokuwa yanaandaliwa na wafanyakazi wa shule,wakati wa hafla za mwishoni mwa mwaka na katika mashindano mengine ya jumuiya akiwakilisha shule yake.
Ingawa amekulia katika familia ya Kiislamu yenye wasichana sita na wavulana wawili, Zari hakuacha mapenzi yake kwenye muziki. Alianza muziki akiwa na umri mdogo na albamu yake ina nyimbo kali kama ‘Toloba’ na ‘Hotter Than Them’. Watu waliomvutia katika muziki ni Wasanii wa Marekani Arethal Franklin na Whitney Houston wakati akiwa sekondari.
Afrika waliomvutia akapenda muziki ni wanamuziki wa Afrika Kusini Brenda Fassie, Miriam Makeba, Lucky Dube na Malkia wa Muziki Afrika Kusini, Yvone Chaka Chaka. Alipojiunga na sekondari alijiunga na makundi ya dansi,drama na muziki jambo ambalo lilimsaidia kuchaguliwa kwa miaka miwili mfululizo la Muigizaji Bora.
Baada ya miaka miwili ya kufanya vizuri katika majukwaa na matamasha ya shule, alipumzika na kuhama kutoka Uganda kwenda London, Uingereza na kuendelea na masomo yake lakini bado mapenzi yake kwa muziki yakiwa mawazoni mwake. Zari kwa msaada wa familia, mashabiki na marafiki wa- naopenda mtindo wa muziki wake na kuamini anaweza aliamua kuchukua hatua mwaka 2007 wa kurekodi singo yake ya kwanza inayoitwa Oliwange (ikiwa na maana wewe ni wangu) .
Mwaka 2008 Zari alishinda Tuzo ya Channel O ya Video Bora ya Muziki ya Msanii Bora Afrika Mshariki. Hafla ya tuzo hizo ilifanyika Johannesburg, Afrika Kusini. Tangu hapo Zari ameendelea kutoa nyimbo zaidi za kuvutia, huku akitiwa moyo na mashabiki wake wakati huo.
Mwaka 2009 alipata Tuzo inayojulikana kama Diva ya mwaka katika kipengele cha Diaspora tangu hapo aliendelea kutengeneza muziki. Zari hivi sasa anaishi Afrika Kusini ambapo anamiliki maduka makubwa ya vipodozi na shule ya elimu ya juu mjini Pretoria wakati akiendelea kujijenga kimuziki.
Inaelezwa kuwa Zari na aliyekuwa mumewe Ivan wanamiliki Shule ya Brooklyn City ambayo ina kampasi sita Afrika Kusini, huku kila moja ikiwa na wanafunzi kati ya 800 hadi 2,100. Wanafunzi hao hupewa vyeti vya taifa wanapomaliza mwaka. Vile vile Zari amejenga hosteli iliyopo barabara ya Sir Apollo Kaggwa, Kampala na anamiliki nyumba kadhaa katika mji huo hasa eneo la Munyonyo, pamoja na duka kubwa la nguo Afrika Kusini.
Ingawa muziki wake haujafanya vizuri kama wanamuziki wengine wa Uganda akiwemo Jose Chameleone, Bebe Cool, Bobi Wine na Ragga Dee, Zari amekuwa akifurahia kwa mafanikio zaidi kwenye biashara na kutokana na hilo anasema lazima arudishe kwa jamii na hivyo kuamua kusaidia vituo na taasisi kadhaa zinazohitaji misaada kama Katalemwa Cheshire Home, Sanyu Babies’ Home pamoja na Gereza la Luzira.
Mfano mwaka 2013 kutokana na moyo wake wa kusaidia,kwa kutimiza hilo baada ya sherehe zake anazozifanya kila mwisho wa mwaka aliamua kutembelea Kituo cha Watoto Yatima cha M-Lisada kilichopo Nsambya siku moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi, akifuatana na watoto wake Pinto, Didy na Quincy.
Alitoa zawadi maalum kwa watoto hao, ambapo Zari alishiriki kuandaa chakula cha Krismasi na kisha baadaye wanawake, sukari, biskuti, mchele na matoke. Mbali na masuala mengine yote, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali,watu wengi nchini Uganda wanakubaliana kuwa Zari ndio Mwanamke Mrembo zaidi nchini humo.
“Sitafuti umaarufu, wenyewe umaarufu ndio hunifuata,”aliwahi Zari kusema kupitia mtandao wa Red Pepper akikanusha habari za baadhi ya watu wanaodai kuwa anatafuta umaarufu kwa nguvu.
Habari zake kuandikwa katika mitandao ya kijamii pamoja na shughuli zake za uhisani zimesababisha wengi kudai kuwa anataka tu umaarufu, kujulikana na kuzungumziwa kila wakati.Hata hivyo akijibu madai hayo, Zari alisema umaarufu unamtafuta yeye na sio kwamba yeye anautafuta.
ConversionConversion EmoticonEmoticon