10 2015 MAMA KANUMBA AMTUHUMU LULU MAZITO, LULU NAE AJIBU MAPIGO BILA AIBU


Staa wa sinema za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

HALI ni mbaya! Staa wa sinema za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mama wa aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba, Flora Mtegoa wamefikia pabaya baada ya mama huyo kumshushia Lulu maneno makali na ya shutuma, Amani lina taarifa.

Habari zilizojiri ndani ya chumba cha habari cha gazeti hili zinadai kuwa, mama Kanumba amemlalamikia Lulu kwamba, amemtupa na kumtenga tofauti na zamani ambapo uhusiano wao ulikuwa kama wa mama na binti yake.

“Jamani habari nzito kwa sasa ni mama Kanumba na Lulu. Mama Kanumba anamshutumu Lulu kwa kumtenga. Anasema ni miezi mitano sasa Lulu hajafika nyumbani kwake wala kuwasiliana naye kwa simu,” kilisema chanzo kimoja.

Kikaendelea: “Hivi kesho (Jumanne iliyopita), ni Kanumba Day. Imepangwa kufanyika Dar West (Dar), inawezekana Lulu asiende au Mama Kanumba asiende. Lakini hata kama watakwenda na wakakutana, watachekeana kwa jino pembe lakini uhusiano wao si mzuri jamani.”

Mama Kanumba akilia peke yake kaburini.

MAMA KANUMBA ATAFUTWA
Ili kupata usahihi wa madai hayo, Amani lilimsaka mama Kanumba kwa njia ya simu ambapo alipopatikana alikuwa na haya ya kusema:“Lulu si Lulu yule jamani. Lulu sasa hivi amebadilika. Awali aliniambia hatanitupa, lakini sivyo. Lulu siku hizi haji kunisalimia wala hanipigii simu.”

ANACHOAMINI YEYE
“Imefika mahali nawaza kwamba, huenda alipenda Kanumba aondoke ili yeye apate mafanikio makubwa aliyonayo sasa. Lulu amenitenga, amenitenga, amenitenga!”

MANENO YA MAMA KANUMBA KABURINI KWA KANUMBA
Juzi, Jumanne, ambayo ilikuwa siku ya kuadhimisha mwaka wa tatu tangu kifo cha staa huyo, mama huyo alishiriki kwa kwenda kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar kwa lengo la kusafisha kaburi la mtoto wake. Baada ya zoezi la kusafisha kaburi kumalizika, mama Kanumba aliongea na Amani na kuyasema haya:

“Nasikitika sana namna ambavyo Lulu amekuwa tofauti na maneno yake ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi katika kuadhimisha kumbukumbu ya Kanumba. Lakini leo kama hivi, hajatokea.
“Pia nasikitishwa na kitendo cha kufanya bethidei ya mdogo wake jana (Jumatatu usiku) kule Posta wakati anajua ndiyo usiku ambao Kanumba alifariki dunia.

Mama Kanumba akiwa na simanzi kubwa.

“Mbaya zaidi, akiulizwa na watu kwa nini sasa hivi hayupo sambamba na mimi kama zamani, anajibu majibu ambayo hayaeleweki. Kumbe maneno yake ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi yalikuwa ya usaliti.

“Kwa hiyo na mimi sasa nimeamua kubaki peke yangu kama nilivyo, nitaendelea kumuenzi Kanumba mwanangu kwa sababu mimi ndiyo mama yake kwa hiyo nalia peke yangu.”

LULU ALITOA AHADI YA UONGO
Katika mazungumzo yake, mama Kanumba alikwenda mbali zaidi kwa kusema: “Kuna siku aliahidi kwamba atajengea picha ya Kanumba ikiwa ndani ya kioo na kuiweka juu ya kaburi, hajafanya hivyo. Nitafanya mwenyewe.“Labda amepuuza kwa vile anajiona anazidi kukua kisanii, ni supastaa ndiyo maana anatoa ahadi za uongo.”

ALICHOKISEMA LULU SASA
Lulu alipotafutwa juzi ili kuzungumzia malalamiko ya mama mkwe wake huyo, hakupatikana lakini wiki iliyopita alizungumza na paparazi wetu kuhusu mtazamo wa maisha yake kwa jumla ambapo alisema:“Mimi kwa sasa hivi nina mtazamo mwingine kabisa kuhusu maisha. Kwanza sidhani kama nitamwaga machozi tena kuhusu Kanumba maana nimelia sanasana.“Mtu ambaye naweza kumlilia ni mama yangu (Lucresia Karugila) na mdogo wangu. Lakini si mtu mwingine. Kwa sasa naangalia zaidi familia yangu.”

Marehemu Steven Kanumba enzi za uhai wake.

TUJIKUMBUSHE KIDOGO
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 kwa kuanguka katika mazingira yaliyodaiwa yalitokana na ugomvi kati yake na Lulu. Tukio hilo lilitokea nyumbani kwa Kanumba, Sinza ya Vatcan, Dar.
Baada ya kifo hicho, Lulu alikamatwa na kuwekwa mahabusu ya Segerea jijini Dar na baadaye kuachiwa kwa dhamana.

Baada ya kutoka mahabusu, yeye na mama yake walimfuata mama Kanumba na kuomba msamaha ambapo mama huyo aliupokea na kusema anamwona Lulu kama mtoto wake na yote ya nyuma yamepita. Kuanzia hapo, Lulu na mama Kanumba wamekuwa na ukaribu wa kindugu huku kila mwaka wakifanya kumbukumbu ya Kanumba pamoja.

Katika kumbukumbu ya juzi, Lulu hakutokea na mama Kanumba alisema hajapewa taarifa yoyote. Lulu alipotafutwa kwa simu ili kumsikia anasema nini kuhusu kutotokea makaburini, hakuwa hewani!
Previous
Next Post »