NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SIKU
chache baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
kukamatwa na kuhojiwa na polisi na hatimaye kuzimia, utata mpya umeibuka
juu ya kiongozi huyo wa kiroho.
Utata
huo unahusu uraia, historia yake, utajiri na umiliki wa silaha ambayo
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linadai haina kibali huku
yeye akidai ana vibali vyote.
Hali hiyo imeibuka huku nyuma ya pazia kukiwa na sintofahamu juu ya hatima yake.
Ingawa
Askofu Gwajima, amelazwa Hospitali ya TMJ kwa siku ya tano leo, bado
anaendelea kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi
ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo.
AHOJIWA KWA STAILI YA FBI
Baada
ya kujisalimisha polisi Machi 27, mwaka huu, Askofu Gwajima anadaiwa
kuhojiwa kwa staili ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Inaelezwa
alihojiwa na makachero tofauti waliokuwa wakipishana katika chumba cha
mahojiano na ambao wanaonekana kubobea katika taaluma hiyo.
Wakati
akidhani mahojiano yamemalizika, inadaiwa waliingia maofisa wengine
kumhoji maswali tofauti tofauti, mtindo ambao unatumiwa zaidi na
wapelelezi wa FBI.
Hatua
hiyo, pia inadaiwa kuchangia kuzimia kwake ambapo awali alidhani
mahojiano yangekuwa ni kuhusu kumkashifu Kardinali Pengo tu.
KULAZWA HOSPITALI
Kabla
ya kulazwa katika Hospitali ya TMJ, Askofu Gwajima alipelekwa katika
Hospitali ya Polisi Kurasini na baadaye Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) ambapo yeye na wafuasi wake waligoma na kutaka atibiwe TMJ ambapo
kuna daktari wake maalumu.
URAFIKI NA WANASIASA
Askofu
Gwajima, kwa muda sasa amekuwa rafiki wa wanasiasa mbalimbali nchini
wakiwamo wa vyama vya upinzani, chama tawala, wastaafu pamoja na baadhi
ya mawaziri walioko ndani ya Serikali ambao hukutana faragha, hadharani
na wengine hushiriki katika ibada kanisani kwake.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani tayari wamemtembelea hospitalini alikolazwa.
UTATA SAKATA LA DK. ULIMBOKA
Sura
ya pili ya Askofu Gwajima, ilianza kuonekana mwaka 2012, baada ya
kanisa lake kuingia katika utata na sintofahamu baada ya kijana
aliyedaiwa kumteka na kumtesa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk. Steven Ulimboka kukamatwa na polisi.
Polisi
walimkamata kijana huyo kwa kile kilichodaiwa kujisalimisha kwenye
kanisa la Askofu Gwajima ambalo alikwenda kutubu kosa la kumshambulia
Dk. Ulimboka.
Mtuhumiwa
huyo, Joshua Mlundi, raia wa Kenya alikiri kuhusika kumteka na kumtesa
Dk. Ulimboka akiwa na wenzake 12 waliokodiwa na mtu aliyehisi anatoka
serikalini.
Hata
hivyo, Askofu Gwajima alisema Mlundi hakwenda kanisani hapo kutubu,
bali alitaka kumuona kiongozi huyo wa kiroho baada ya kumweleza kuwa
alikuwa na tatizo la kuropoka.
MAISHA YA KITAJIRI
Askofu Gwajima ni kiongozi wa kiroho mwenye ukwasi pengine kuliko wote nchini.
Anadaiwa
anamiliki helikopta yake mwenyewe, gari la kifahari aina ya Hummer
lenye thamani ya Sh milioni 250 na nyumba ya ghorofa nne maeneo ya Mbezi
Beach, jijini Dar es Salaam.
Pamoja
na kumiliki vitu hivyo, Askofu Gwajima amewanunulia wachungaji wake
magari 30, kila mmoja gari zuri la kutembelea wakati wa kueneza injili.
Pia, amewanunulia waumini wake mabasi 20 ya kuwapeleka kanisani na kuwarudisha makwao siku za ibada na wakati wa maombi maalumu.
Pia anamiliki shamba la mifugo wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Katika
kanisa lake, Askofu Gwajima amefunga spika maalumu zenye nembo ya ‘JG’
yaani Josephat Gwajima ambazo amezinunua nchini Marekani kwa oda
maalumu.
KAULI TATA ZA GWAJIMA
Mwaka
jana wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Dengue, Askofu Gwajima alikaririwa
akisema hakuna ugonjwa kama huo isipokuwa umetengenezwa ili watu
wajipatie fungu kutoka serikalini.
Alisema
mbu aina ya Ades anayeeneza ugonjwa huo, alikuwapo tangu siku nyingi
lakini hakuwa na madhara hadi baadhi ya viongozi ambao hakuwataja
walipoutangaza na kuwalipa watu ili watangaze wameambukizwa ugonjwa huo.
URAIA NA HISTORIA YAKE
Suala
la uraia wa Askofu Gwajima limekuwa mjadala kwa baadhi ya Watanzania,
wakionyesha shauku ya kutaka kujua historia ya maisha yake.
Vyanzo
mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamiii ya ‘twitter’, ‘facebook’ na
tovuti yake, vimebainisha kuwapo kwa sintofahamu nyingi kuhusu asili
yake.
Katika
tovuti yake, Askofu Gwajima ambaye alianzisha kanisa lake mwaka 1994,
hakutaja jina la kijiji alichozaliwa ingawa anasema alizaliwa mwaka 1970
mkoani Mwanza.
Katika
tovuti yake hiyo, ameelezea historia yake akisema ni mtoto wa 12 katika
familia yao ambayo iliishi katika kijiji ambacho hakikuwa na kanisa.
Anasema katika tovuti yake kuwa alipatwa na maradhi ya kupooza akiwa na umri wa miaka 10.
Alitaja
sababu iliyosababisha apooze kuwa ni ajali ambayo hakuibainisha ni ya
aina gani, ingawa anasema alikaa kitandani kwa muda wa miaka sita na
kupoteza matumaini ya kupona.
Hali
hiyo, anaelezea ilisababisha madaktari wathibitishe kuwa asingeweza
kurejea katika hali yake ya kawaida, lakini alipona baada ya kutokewa na
Yesu na kumponya hali iliyomfanya ampe maisha yake kuanzia siku hiyo.
Kuhusu
elimu yake, askofu huyo anasema amesomea masuala ya Biblia jijini
Nairobi nchini Kenya katika shule ya East Africa Pastorial Theological.
Hata hivyo, hajaeleza kiwango chake cha elimu alichopata.
Baada
ya kuhitimu alianza kufanya kazi ya kumtumikia Mungu ambapo alifungua
kanisa katika Jiji la Mwanza, mji mdogo wa Mugumu uliopo Serengeti,
Musoma na Dar es Salaam.
Kwa sasa anaongoza makanisa mengi ndani na nje ya Tanzania.
Gwajima ni mume wa mchungaji Grace ambaye amezaa naye watoto watatu ambao ni Ruth, Freeman na Manase.
Amefanikiwa
kuhubiri katika nchi mbalimbali za Afrika, Marekani, Uingereza, Uswisi,
Japan, Korea Kusini, Ujerumani, China na nyinginezo.
Askofu
huyo ambaye amejipatia sifa kutokana na staili yake anayodai kwamba
anafufua wafu, alitangaza kupata Shahada ya Uzamivu (Phd) kutoka Chuo
Kikuu cha Omega Global nchini Afrika Kusini na sherehe yake ilifanyika
Hoteli ya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
KAKA YAKE AJITOKEZA
Methusela
Gwajima, aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wa Askofu Gwajima amejitokeza
na kusema kuwa asili yao ni Kijiji cha Koromije Kwimba, Mwanza.
Alisema
kwa sasa familia ya mchungaji huyo ipo jijini Mwanza eneo la Mkolani
ambako alisema yuko mama yake mzazi na baba yake yuko jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya matibabu.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Methusela alisema ingawa
mdogo wake anaumwa, lakini anamtaka amwombe radhi Kardinali Pengo kwa
njia alizozitumia kuwasilisha ujumbe wake wakati akimchafua.
MADAI YA KUTOROSHWA
Juzi,
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova
alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akidai kukamata watu 15 wakitaka
kumtorosha Askofu Gwajima.
Kamanda Kova alidai watu hao walifika hospitalini saa 9:30 usiku kwa lengo hilo.
Alisema
walipekuliwa na kukutwa na begi ambalo lilikuwa na bastola aina ya
Berreta yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za shotgun
na vitabu viwili vya hundi za benki.
Vitu
vingine ni hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Josephat Mathias
yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi cha Benki ya Equity pamoja na
nyaraka mbalimbali za Kampuni ya Puma, chaja ya simu, tablets, suti
mbili na nguo za ndani.
GWAJIMA AIBUKA
Jana, Askofu Gwajima alivunja ukimya baada ya kukanusha taarifa za yeye kudaiwa kutaka kutoroshwa na wafuasi wake 15.
Alisema
bastola iliyokutwa katika begi lililochukuliwa wodini kwake, anaimiliki
kihalali kwa ajili ya kujilinda na si vinginevyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari wodini alikolazwa, Askofu Gwajima alisema
ameshangazwa na taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari kwamba
wafuasi wake walitaka kumtorosha.
“Juzi
baada ya kupata taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa
nimefariki dunia, maaskofu wenzangu walikuja kuniona na kunishauri
niachane na taarifa hizo huenda zilikuwa na lengo maalumu.
“Baadaye
nikawaambia wachungaji wangu waende nyumbani kwangu na kuchukua begi
lililokuwa chumbani ambapo ndani yake palikuwa na baadhi ya nguo pamoja
na bastola na nyaraka za umiliki wa silaha hiyo pamoja na vitu vingine.
“Walifikisha
begi na kuliweka hapa wodini nilikolazwa, lakini walitokea watu ambao
walijitambulisha kuwa ni askari na kuomba mzigo ulioingizwa ndani na
hapakuwa na ushindani nikawapa,” alisema Askofu Gwajima.
AZUNGUMZIA KUZIMIA KWAKE
Akizungumzia
kuzimia kwake alipokuwa akihojiwa na polisi, alisema awali alitoa
taarifa kwa askari hao kwamba alikuwa anaumwa kichwa, lakini
hakusikilizwa wala kupatiwa huduma yoyote.
Hata hivyo, alisema hana mgogoro wowote na Kardinali Pengo na kwamba kilichotokea alikuwa katika kazi yake ya kukemea.
TAARIFA MBILI ZA KAMANDA KOVA
Awali Kamishna Kova alisema bastola yenye namba CAT 5802 iliyokutwa kwenye begi la Askofu Gwajima haina umiliki wa mtu yeyote.
Alisema
kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili
kubaini kwanini Askofu Gwajima alikuwa akimiliki silaha kinyume cha
sheria.
Alisema wanasubiri atoke hospitali ili waendelee kumhoji zaidi.
Baadaye
jana jioni, Kova alituma taarifa nyingine kwa vyombo vya habari akisema
uchunguzi wa kina na wa kitaalamu umethibitisha silaha hiyo inamilikiwa
kihalali na Askofu Gwajima.
Alisema risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun yenye namba 102837 zinamilikiwa kihalali.
MAASKOFU KUMWONA IGP
Katika
hatua nyingine, maaskofu na wachungaji kutoka makanisa ya Kipentekoste
zaidi ya 100 leo wanatarajia kwenda kumwona Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP), Ernest Mangu ili kujadili suala la Askofu Gwajima.
Akisoma
tamko hilo kwa niaba ya wenzake, Askofu Damasi Mukassa kutoka Dodoma
alisema wanakwenda kumwona IGP Mangu kwa ajili kuwataka watumie weledi
na uadilifu kushughulikia suala hilo
ConversionConversion EmoticonEmoticon