TANZANIA imetajwa kuwa kinara katika
nchi za Afrika Mashariki kwa kutunza amani na utulivu tangu ipate uhuru,
huku Rais Jakaya Kikwete akiibuka kiongozi bora katika ukanda huo kwa
kujitolea kuleta amani katika Bara la Afrika na kutunza amani hiyo
nchini mwake.
Kwa hali hiyo, Rais Kikwete ametunukiwa
tuzo mbili na Taasisi ya East Africa Book of Records ya nchini Uganda,
moja ikiwa ni kwa ajili ya Tanzania ambayo imefanikiwa kutunza amani
pamoja na utulivu tangu uhuru na nyingine ni ya Rais Kikwete mwenyewe
kutokana na juhudi zake za kupigania amani nchini mwake na eneo lote la
ukanda wa mashariki mwa Afrika.
Kutokana na tuzo hizo, sasa Rais Kikwete
ameacha kumbukumbu katika vitabu vya nchi za Afrika Mashariki, kama mtu
na kiongozi maarufu aliyetoa mchango mkubwa katika kuleta amani kwenye
nchi za ukanda huu.
Akikabidhi tuzo hizo jana Ikulu, Dar es
Salaam, Kiongozi wa taasisi hiyo Dk Paul Bamutaze alisema wametoa tuzo
hizo baada ya kuangalia mchango wa Rais Kikwete katika kuleta amani
katika baadhi ya nchi barani Afrika, akitoa mfano namna kiongozi huyo
alivyoleta amani mwaka 2008 nchini Kenya, kufuatia machafuko baada ya
kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
“Tuzo ya kwanza tunaitoa kwa Tanzania
kama nchi kwani ndio nchi pekee katika eneo la Afrika Mashariki ambayo
imedumisha amani na utulivu tangu kupata uhuru na ndio imekuwa inasaidia
kutatua migogoro mbalimbali kwa majirani zake na inaendeshwa kwa
utawala wa sheria,” alisema Dk Bamutaze.
Alisema tuzo ya pili wanamkabidhi Rais
Kikwete kutokana na kuwa kiongozi bora, ambaye amedumisha amani nchini
mwake, lakini pia ameshiriki kutatua migororo mbalimbali.
Alisema licha ya Kenya, lakini ni Rais
Kikwete ambaye ameshiriki kuleta amani nchini Burundi na kurejesha
serikali iliyokuwepo madarakani baada ya kuwepo jaribio la uasi.
Rais Kikwete pia amesaidia kuleta amani
katika nchi za Sudan Kusini, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) baada ya Jeshi la Tanzania kuwasambaratisha kundi la waasi la M23.
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa taasisi
hiyo, Adam Buyinza alisema katika utafiti ambao wameufanya, wamegundua
kuwa Tanzania imedumu kuwa na amani kutokana na kuongozwa na CCM ambacho
kina sera zinazoeleweka.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema
kwamba misingi ya amani na utulivu uliopo nchini umewekewa misingi yake
na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye uongozi wake haukubagua watu kwa
misingi ya kidini, rangi na kabila au eneo ambako anatoka mtu.
Alisema tuzo hiyo aliyoipokea sio yake
peke yake, bali ni ya wananchi wa Tanzania pamoja na wasaidizi wake
ambao yeye kama nahodha wa meli wamesaidiana kuhakikisha kuwa meli yao
inaenda vizuri hata pale panapotokea mawimbi wanasaidiana kukiendesha
chombo hicho.
Rais Kikwete alisema kuwepo kwa amani
nchini, kumetokana na watu wake kuamini kwenye majadiliano badala ya
kupigana na alisema hata pale ilipotokea tofauti kati ya Serikali na
vyama vya upinzani, walikaa meza moja wakazungumza na pale ilipotokea
tofauti kati ya Waislamu na Wakristo pia walitatua migogoro yao kwa
mazungumzo.
“Kwa mfano kulitokea ugomvi wa nani ana
uhalali wa kuchinja, haya mambo walitaka mimi niingilie kati, lakini
jamii yenyewe walikaa na kujadiliana kwamba yametoka wapi na nani
ameyachochea, walipokaa waligundua kwamba hakuna faida kwani mambo hayo
wamejiwekea jamii husika,” alisema Rais Kikwete.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, alisema kwamba tuzo hizo alizotunukiwa Rais
Kikwete ni kitu kikubwa kwa Rais anayeondoka madarakani.
ConversionConversion EmoticonEmoticon