Rais Kikwete Ndio Rais Bora Afrika Mashariki..Atunikiwa Tuzo ..Soma Hapa


TANZANIA imetajwa kuwa kinara katika nchi za Afrika Mashariki kwa kutunza amani na utulivu tangu ipate uhuru, huku Rais Jakaya Kikwete akiibuka kiongozi bora katika ukanda huo kwa kujitolea kuleta amani katika Bara la Afrika na kutunza amani hiyo nchini mwake.

Kwa hali hiyo, Rais Kikwete ametunukiwa tuzo mbili na Taasisi ya East Africa Book of Records ya nchini Uganda, moja ikiwa ni kwa ajili ya Tanzania ambayo imefanikiwa kutunza amani pamoja na utulivu tangu uhuru na nyingine ni ya Rais Kikwete mwenyewe kutokana na juhudi zake za kupigania amani nchini mwake na eneo lote la ukanda wa mashariki mwa Afrika.

Kutokana na tuzo hizo, sasa Rais Kikwete ameacha kumbukumbu katika vitabu vya nchi za Afrika Mashariki, kama mtu na kiongozi maarufu aliyetoa mchango mkubwa katika kuleta amani kwenye nchi za ukanda huu.

Akikabidhi tuzo hizo jana Ikulu, Dar es Salaam, Kiongozi wa taasisi hiyo Dk Paul Bamutaze alisema wametoa tuzo hizo baada ya kuangalia mchango wa Rais Kikwete katika kuleta amani katika baadhi ya nchi barani Afrika, akitoa mfano namna kiongozi huyo alivyoleta amani mwaka 2008 nchini Kenya, kufuatia machafuko baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

“Tuzo ya kwanza tunaitoa kwa Tanzania kama nchi kwani ndio nchi pekee katika eneo la Afrika Mashariki ambayo imedumisha amani na utulivu tangu kupata uhuru na ndio imekuwa inasaidia kutatua migogoro mbalimbali kwa majirani zake na inaendeshwa kwa utawala wa sheria,” alisema Dk Bamutaze.

Alisema tuzo ya pili wanamkabidhi Rais Kikwete kutokana na kuwa kiongozi bora, ambaye amedumisha amani nchini mwake, lakini pia ameshiriki kutatua migororo mbalimbali.
  
 Alisema licha ya Kenya, lakini ni Rais Kikwete ambaye ameshiriki kuleta amani nchini Burundi na kurejesha serikali iliyokuwepo madarakani baada ya kuwepo jaribio la uasi.

Rais Kikwete pia amesaidia kuleta amani katika nchi za Sudan Kusini, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya Jeshi la Tanzania kuwasambaratisha kundi la waasi la M23.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa taasisi hiyo, Adam Buyinza alisema katika utafiti ambao wameufanya, wamegundua kuwa Tanzania imedumu kuwa na amani kutokana na kuongozwa na CCM ambacho kina sera zinazoeleweka.

Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema kwamba misingi ya amani na utulivu uliopo nchini umewekewa misingi yake na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye uongozi wake haukubagua watu kwa misingi ya kidini, rangi na kabila au eneo ambako anatoka mtu.

Alisema tuzo hiyo aliyoipokea sio yake peke yake, bali ni ya wananchi wa Tanzania pamoja na wasaidizi wake ambao yeye kama nahodha wa meli wamesaidiana kuhakikisha kuwa meli yao inaenda vizuri hata pale panapotokea mawimbi wanasaidiana kukiendesha chombo hicho.

Rais Kikwete alisema kuwepo kwa amani nchini, kumetokana na watu wake kuamini kwenye majadiliano badala ya kupigana na alisema hata pale ilipotokea tofauti kati ya Serikali na vyama vya upinzani, walikaa meza moja wakazungumza na pale ilipotokea tofauti kati ya Waislamu na Wakristo pia walitatua migogoro yao kwa mazungumzo.

“Kwa mfano kulitokea ugomvi wa nani ana uhalali wa kuchinja, haya mambo walitaka mimi niingilie kati, lakini jamii yenyewe walikaa na kujadiliana kwamba yametoka wapi na nani ameyachochea, walipokaa waligundua kwamba hakuna faida kwani mambo hayo wamejiwekea jamii husika,” alisema Rais Kikwete.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema kwamba tuzo hizo alizotunukiwa Rais Kikwete ni kitu kikubwa kwa Rais anayeondoka madarakani.
Previous
Next Post »