Rais wa Manzese ambaye ni staa wa Bongo Fleva, Hamad Ally ‘Madee’ amelala nyumba ya nondo za mahabusu baada ya kutiwa mbaroni akihusishwa na utekaji wa dereva wa bodaboda, Suedi Waziri (pichani) kisha kumpa kipigo cha mbwa mwizi
Akizungumza na gazeti hili, mmiliki wa bodaboda iliyokuwa ikiendeshwa na Waziri ambaye ni msanii wa filamu na Mkurugenzi wa Hamadombe Distributor, Fatuma Makame ‘Joanita’ alisema tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita ambapo Madee alikuwa akifanya shoo katika Ukumbi wa Kumbia Pub uliopo Vijibweni Kigamboni, Dar.
Kwa mujibu wa shushushu wetu, baada ya Madee kumaliza shoo ukumbini hapo, mashabiki walimsindikiza kwa shangwe ambapo gari lake lilikuwa katika mwendo wa taratibu ndipo Waziri aliyekuwa amempakia abiria nyuma, abiria huyo wake akadaiwa kukwapua simu ya msanii huyo na kutokomea kusikojulikana.
Dereva wa bodaboda, Suedi Waziri anayedaiwa kutekwa na staa wa Bongo Fleva, Hamad Ally ‘Madee’.
Ilidaiwa kwamba Waziri alibaki akiwa amepigwa butwaa baada ya tukio hilo kwani wakati anampakia abiria huyo hakujua ni kibaka ambapo akiwa ameduwaa, alishangaa kupokea kipigo kikali kutoka kwa Madee na wenzake ambapo walimchukua na pikipiki yake wakampeleka hadi nyumbani kwa Madee, Manzese, Dar kisha kumpa mateso kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 8:00 usiku.
Iliendelea kudaiwa kwamba asubuhi iliyofuata akina Madee walimpigia simu mama mdogo wa Waziri na kumtaka apeleke fedha kwa ajili ya kununulia simu kwani mwanaye alikuwa amekwapua simu ambapo mama huyo alifika katika Kituo cha Polisi cha Magomeni, Dar na kutoa taarifa.
Ilisemekana kwamba mama huyo aliwachukua polisi wa difenda kisha akatimba nao Manzese kwa Madee na kumchukua kijana huyo akiwa na maumivu makali kwani alikuwa amechanwa na viwembe lakini wahusika walikimbia.
Joanita aliendelea kusema baada ya hapo, Madee alikwenda kuripoti polisi Magomeni ambao walimwambia anatakiwa akatoe taarifa hizo kwenye Kituo cha Polisi cha Kigamboni kwani ndipo tukio lilipotokea.
Alisema kwamba Madee alifanya hivyo bila ubishi na hapo ndipo aliposwekwa lupango na kulala huko japokuwa jamaa zake walifanya jitihada za kumtoa lakini ikashindikana.
Madee amefunguliwa shitaka katika Kituo cha Polisi cha Kigamboni kwa jalada namba VJB/RB/625/2014
KUTEKWA KWA BINADAMU.
Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni polisi walikuwa wakikagua nyumbani kwa Madee na kuona sehemu ambayo kijana huyo alikuwa akiteswa huku simu ya Madee ikiita bila kupokelewa.
Habari zinadai msanii Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ naye anasakwa na polisi kuhusiana na tukio hilo kwa sababu alikuwa na Madee.
ConversionConversion EmoticonEmoticon