WATOTO 8 WAKUTWA WAMEUAWA NDANI YA NYUMBA AUSTRALIA

Wakazi waishio jirani na eneo la mauaji hayo wakiwa wamekusanyika nje ya nyumba hiyo mjini Cairns.
WATOTO nane wamekutwa wameuawa kwenye nyumba moja katika mji wa Cairns eneo la Queensland kaskazini mwa Australia.
Polisi nchini Australia wakiendelea na uchunguzi katika eneo hilo.
Vyombo vya habari nchini humo vimesema kuwa watoto hao wote kati ya miezi 18 na miaka 15 walikuwa wamechomwa visu.
Polisi wa eneo la Queensland wanasema kuwa waliitwa kwenda kwenye nyumba hiyo baada ya ripoti kutolewa kwamba mwanamke mmoja alikuwa amejeruhiwa vibaya. Lakini ndani ya nyumba hiyo polisi waligundua maiti za watoto nane.
Inaaminika kuwa watoto hao walichomwa visu hadi kufa. Polisi wanasema kuwa mtoto mdogo zaidi kati ya watoto hao alikuwa na umri wa miezi 18 na mkubwa zaidi alikuwa na miaka 15.
Polisi wakiwafariji majirani waliokusanyika nje ya nyumba yalipotokea mauaji.
Mwanamke ambaye anakisiwa kuwa na umri wa miaka 30 amepelekwa hospitalini akiwa na majeraha ya visu. Ndugu mmoja wa familia hiyo aliwaambia polisi kuwa mwanamke huyo alikuwa mama wa watoto hao.
Polisi wanasema kuwa mama huyo hajakamatwa lakini anawasaidia kwa uchunguzi. Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott amekitaja kisa hicho kuwa uhalifu mbaya na pia kuzitaja habari hizo kuwa za kuvunja moyo.
Baadhi ya waombolezaji waliweka maua nje ya nyumba hiyo.
Polisi hawajaweza kuthibitisha ambavyo watoto hao waliuawa hadi pale uchunguzi utakapofanyika.
Wanazungumza na watu kadhaa akiwemo mwanamume aliyeonekana karibu na nyumba hio asubuhi na mapema, ingawa hakuna mtu yeyote amekamatwa.
Previous
Next Post »