EXCLUSIVE: BAADA YA HUKUMU, CHEKA AFUNGUKA KILA KITU

Cheka akikabidhiwa ufunguo wa gari na Meya wa Ilala, Jerry Silaa baada ya pambano ambalo mshindi alipewa gari.
“BONDIA mahiri wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka amehukumiwa kifungo cha kwenda jela miaka mitatu kutokana na kumshambulia aliyekuwa meneja wa baa yake, Bahati Kibanda ‘Masika’ tukio ambalo lilitokea Julai 2, mwaka jana...”
Polisi (kushoto) akimwamuru Cheka kutoongea na simu.
Hiyo ilikuwa ni ‘breaking news’ katika kituo cha redio cha E-FM, Jumatatu ya wiki hii, mara baada ya kusikia hivyo haraka tukakumbuka kuwa Cheka alikuwa na kesi dhidi ya meneja huyo, lakini kwa kuwa tukio lenyewe lilitokea zamani, kumbukumbu ya kesi itasomwa lini ilipotea, haraka tukaamua kupiga simu kwenye namba ya Cheka mwenyewe.

(Simu inaita, baada ya muda mfupi ikapokelewa). “Haloo.”

Cheka akiwa na baadhi ya mikanda yake ya ubingwa.
Championi: Mambo vipi, nazungumza na Francis Cheka?
Cheka: Ndiyo, ni mimi kaka, niambie.

Championi: Pole sana kwa matatizo, tumepata taarifa kuwa umehukumiwa kwenda jela miaka mitatu, ni kweli?
Cheka:  Nimeshapoa, ndiyo hivyo kama mlivyosikia ndugu zangu.

Championi: Sasa hapo upo wapi wakati hukumu imeshatoka?
Cheka: Nipo hapahapa katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, nasubiri kuchukuliwa kupelekwa kwa mkuu wa magereza kwa ajili ya kupangiwa gereza.

Championi: Hakimu gani ambaye ametoa hukumu yako?
Cheka: Kama sijakosea anaitwa Said Msuya ni Hakimu Mkazi Mwandamizi.

Kwa hiyo tunaweza kuendelea kuzungumza?
Cheka: Yaaa kaka tuendelee tu kuzungumza.
Nini kilichotokea mpaka ukakumbana na hiyo kesi?
Cheka: Kama utakuwa unakumbuka  mwaka 2012 nilipigana na bondia kutoka Malawi, Chimwemwe Chiotcha kuwania mkanda wa IBF Afrika kule Arusha, kwenye pambano hilo nilipata shilingi milioni tano, ambapo kazi ya hizo, milioni mbili na nusu nikaamua kufungua baa, nyingine iliyosalia nikaitumia kwenye matumizi yangu binafsi.

Baa hiyo inaitwa Vijana Social ipo maeneo ya Sabasaba, nilimkabidhi dada mmoja anaitwa Bahati Kibanda maarufu kwa jina la Masika ili awe msimamizi.

Wakati mimi nikiwa bize na mambo mengine, mauzo yakawa hayaridhishi, sasa katikati ya mwaka jana nikaamua kwenda kuchukua funguo za ofisi hiyo kwa sababu mambo hayakuwa yakienda vizuri.

Akakataa kutoa funguo, kukatokea ubishi kati yetu na hakunipatia funguo. Nikaamua kuondoka eneo hilo, baada ya pale ndipo nikaja kukamatwa kwa madai ya kumshambulia huyo Bahati.

Nikapelekwa polisi, nikatolewa kwa dhamana na baada ya hapo ndipo mlolongo wa kesi ukawa unaendelea mpaka kufikia hatua hiyo ya kuhukumiwa miaka mitatu.

Unazungumziaje hukumu ya kesi yako?
Kiukweli sina cha kusema kwa sababu kesi imeendeshwa katika msingi ambayo mimi sikuridhika nayo, kwani ukweli ni kwamba sikuwahi kumpiga meneja wangu.

Naumia sana lakini hakuna anayejua maumivu yangu kwa sababu kuna mambo mengi yamejificha wakati wa uendeshaji wa kesi yenyewe, mfano sikuwahi kuambiwa nipeleke shahidi kama inavyotakiwa, kitu kinachonifanya nihisi kuwa hakimu pengine alikuwa anatafuta umaarufu wa kunihukumu.

Mimi sina kawaida ya kupigana nje ya ulingo kwa sababu naheshimu kazi ya mikono yangu, lakini sina jinsi kwa kuwa kuna kikundi cha watu wachache ambao hawapendi kuona Cheka akipata mafanikio, wamechangia katika hili.

“Ninaamini kuwa pengine kitendo cha kudai bati kwa viongozi wa Serikali ya Morogoro ambazo niliahidiwa na Rais Jakaya Kikwete baada ya kushinda pambano langu dhidi ya Phil Williams wa Marekani, kimechangia maana walikuwa  wakinizungusha.

Una mpango wa kukata rufaa?
Binafsi sifikirii kukata rufaa, wewe acha tu niende nikaitumikie adhabu ambayo ilishapangwa na watu wasionipenda eti kwa sababu ya kudai jasho la kazi ya mikono yangu, hawajui ni kiasi gani nilivyoweza kupata ile fedha ya mtaji wa biashara.

Nadhani ndugu zangu pamoja na mashabiki wanaweza kufanya hivyo ila siyo mimi, kwa upande wangu miaka mitatu siyo mingi, najua itaisha tu halafu nitatoka, sina cha kuhofia kwa sababu sikuanza mimi kwenda gerezani.

Una neno gani kwa mashabiki wako?
Waendelee kuniombea huko niendako, kwa sababu nitarejea kwa uwezo wa Mungu, fitina za watu wachache zisiwakatishe tamaa.

Vipi kuhusu biashara yako ya kuokota chupa za maji?
Nadhani ndiyo hivyo imeshakosa mtu wa kuweza kusimamia kwa sababu mke wangu ni mjamzito, hivyo hataweza pilikapilika za kwenda barabarani kuokota chupa, ni jambo gumu sana kwa kweli, naumia lakini sina jinsi.

Mambo yangu mengi yatakufa kwa sasa, kwa sababu mwenyewe sitakuwepo uraiani.

Mwana naona jamaa wamekuja kuninyanyua ndiyo naelekea kupanda gari kuelekea kwenye makazi yangu mapya ambapo nitakuwepo huko kwa miaka mitatu, ila fanya hivi…(akawa azungumzi ila simu ipo hewani)

Championi: Haloo! Haloo! Cheka bado upo hewani? (upande wa pili kimyaa, ila simu ipo hewani, baada ya muda ikakatwa)

Championi: Baadaye kupitia runinga ilionekana kumbe Cheka alikuwa akizungumza na sisi muda huo mpaka alipokaribia kupanda kwenye gari, ndipo askari wakamnyang’anya simu na kumtaka apande. Safari ikaanza kuelekea gerezani.

Baada ya hapo, mkewe, Tosha Azenga aliyekuwa mahakamani aliangua kilio kikubwa, tukaamua kumwacha atulie kwa siki mbili, kisha juzi tukawasiliana naye na mazungumzo yetu yalikuwa hivi:

Ulijisikiaje baada ya hukumu kutolewa?
Binafsi sikuamini kile alichokisema hakimu, niliishiwa nguvu kabisa, kwa sababu ya uchungu, adhabu aliyopewa ni kubwa sana hata kama amekosea.

Umejipangaje baada ya hicho kilichotokea?
Kiukweli maisha yatakuwa magumu sana kwa upande wangu, maana Fransic ndiye alikuwa nguzo ya familia, mimi ni mjamzito na sina uwezo wa kufanya kazi ngumu, pia nina mtoto anaitwa Heshima anayesoma shule ya msingi.

Utaendeleza biashara yake ya baa?
Mimi sijui vizuri kuhusu hiyo biashara yake kwa sababu muda mwingi tulikuwa tunafuatilia kesi.

Vipi kuhusu bati alizoahidiwa?
Alikuwa akifuatilia tangu Joel Bendera alipokuwa mkuu wa mkoa huu (Morogoro) na hata baada ya Bendera kuhamishwa hakupewa hizo bati zenyewe.
   
Una neno gani kwa jamii?
Naomba serikali itusaidie, angalau wangemfunga hata kifungo cha nje, kwani sisi wote akiwemo baba yake mzazi ambaye ana matatizo ya macho tunamtegemea yeye.

Previous
Next Post »