NIMEKOSA NINI?
Alfajiri na mapema niliamka.
Sikuamka kwa bahati mbaya muda huo bali ilikuwa ndiyo kawaida yangu kila siku.
Nilikuwa nikiamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kwenda katika mihangaiko yangu
ya kila siku.
Ingawa siku hiyo nilikuwa kwenye mtoka kisha
nikachelewa sana kurudi nyumbani, sikuwa na budi ya kujidamka asubuhi na mapema
ili niende kazini.
Baada ya kupiga mswaki niliingia maliwatoni
kujiswafi. Nilipomaliza nilirudi chumbani kwangu, nikauramba kama ilivyokuwa
ada kila nilipokuwa naelekea kazini.
Nilichukua suruali yangu niliyokuwa nimevaa jana yake
nilipokuwa kazini ili nichukue pochi iliyokuwa kwenye mfuko wa suruali hiyo
kwani humo ndiyo kulikuwa na nauli yangu ya kunipeleka kazini na kunirudisha
nyumbani.
“Umeiona pochi yangu mama Chris?” Nilimuuliza mke
wangu aliyekuwa kajilaza kitandani kwa wakati huo.
“Hata sijaiona, kwani
ulikuwa umeiweka wapi?” Aliuliza.
“Nakumbuka jana nimeenda
nayo kazini, lakini nimeangalia kwenye suruali niliyokuwa nimevaa sijaiona.”
“Mh! Sasa itakuwa wapi?”
“Kama vipi achana nayo kwa
sasa, acha niende kazini nikirudi nitakuja niitafute vizuri! Cha kufanya sasa
hivi nipe shilingi elfu kumi kwa ajili ya nauli.” Niimwambia mke wangu naye akainuka
na kunichukulia kwenye droo ya kitanda kisha akanipatia.
Nilimuaga mke wangu kwa kumbusu kwenye paji la uso
kisha nikamalizia kwa mwanangu kipenzi aliyekuwa bado kalala.
“Kila la heri mume wangu,
nakutakia kazi njema!” Yalikuwa ni maneno ya mke wangu kipenzi mama Chris,
maneno ambayo alikuwa akiniambia kila
siku nikiwa naelekea kazini.
“Asante mama, na wewe
nakutakia siku njema, utamsalimia mwanangu Chris atakapoamka.” Nilijibu huku nikichana
chana nywele zangu huku nikijiangalia kwenye kioo kikubwa kilichokuwepo kwenye
meza ya kujirembea iliyokuwemo humo chumbani.
Nilipoanza
kuondoka mama Chris akanishika mkono,
“Ngoja kwanza baba
wewe!” Alitamka maneno yale wakati
akiuvuta mkono wangu!
“Nini tena mama?” Nilihoji
kwa lugha ya kubembeleza nikidhani kuwa labda mama Chris anataka mambo yetu
yale ya mchezo wa kikubwa, maana katika kumbukumbu zangu usiku huo timu zote
zilikuwa kambi kwani mwenzangu alikuwa katika sherehe zake za kila mwezi.
“Hii tai haijakaa vizuri mume wangu, angalia na hii
kola ya shati lako shingoni ilivyokaa shaghala baghala, utaenda unachekwa njia nzima!” Aliongea wakati akinirekebisha huku
tabasamu lake mwanana akilitoa.
“Nitachekwa mimi au
utachekwa wewe mke wangu maana umeshindwa kunikagua wakati natoka!”
“Mimi sitachekwa sababu sitakuwepo huko.” Aliongea mke wangu
huku akihamia kwenye tai kuiweka sawa.
Alipomaliza kuyaweka sawa mavazi yangu nilimkumbatia
tena kwa mara nyingine na kumpiga mabusu motomoto kisha nikatoka zangu.
Nilienda mpaka stendi kugombania daladala, si unajua tena usafiri wetu wa huku
Bongo.
Sikuchelewa kupata gari, nikapanda na kwenda kushukia
posta mpya kisha nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea ofisi yetu ilipokuwa.
Nilipofika ofisini nilipigwa na butwaa baada ya
kuwakuta watu wamejazana. Kwa haraka haraka nikaanza kuhisi kuwa kuna tukio
kubwa ambalo lilikuwa limetokea. Watu walikuwa wameuzunguka mlango huku polisi
wakiwa wanarandaranda.
Maswali mia mia yakaanza kuzunguka katika akili yangu
bila kupata majibu. Kwa kuwa nilikuwa tayari nipo kwenye tukio lenyewe,
nilipiga moyo konde na kujiambia kuwa muda si mrefu nitakijua kilichojili.
“Halafu linaonekana ni tukio kubwa sana, yaani mpaka
polisi wamekuja!” Nilijiwazia huku nikitembea kwa tahadhari kuelekea ofisini.
ITAENDELEA........
ConversionConversion EmoticonEmoticon